Thursday, 3 July 2014

WAJUMBE TADEA WAACHWA KWENYE MATAA DAR


Na Linah Mvungi
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa chama cha Tadea kutoka mikoa mbalimbali wameushutumu uongozi wa chama hicho kwa kuwatelekeza baada ya kumalizika kwa kikao hicho cha juu na kuwafanya waishi maisha magumu jijini Dar es Salaam.

Wajumbe hao walihudhuria mkutano wa uchaguzi wa viongozi watakaokiongoza chama hicho kwa kipindi cha miaka saba, katika uchaguzi unaoelezwa kutawaliwa na mizengwe na kutokuwa na ushindani katika nafasi zote za uongozi.

Wajumbe hao walidai kuwa waliahidiwa kurejeshewa nauli baada ya kufika Dar es Salaam, lakini hadi sasa hawajarejeshewa fedha hizo, wakati nauli za kurudi makwao zilitolewa pungufu.

Wanachama hao walilieleza gazeti hili kuwa wamelipiwa malazi pekee bila kupewa fedha zozote za kujikimu. Alipotakiwa kujibu tuhuma hizo, rais wa Tadea, Lifa Chipata alijibu kwa mkato akisema: “Uchaguzi ulikuwa mzuri sana... kwanza wewe mwandishi nani kakwambia uje hapa? Hatujakuita ondoka, kama unaona hawana nauli au wanalalamika waulize wao.”

Wajumbe hao waliofikia Jeshi la Wakovu, Kurasini Dar es Salaam walisema kwa siku mbili mfululizo tangu Jumatatu hadi juzi wamekuwa wakipatiwa mlo mmoja bila hata maji ya kunywa.

Kutoa mizigo

Mjumbe kutoka mkoani Tabora, Michael John alisema juzi uongozi wa Jeshi la Wakovu uliwataka kutoa mizigo nje kutokana na muda waliopangiwa kuishi hapo, kuisha.

“Tuliambiwa tutoe mizigo yetu nje na tulipomwambia Chipata atupatie nauli tuondoke tangu Jumatatu, hakuwa na jibu linaloeleweka na hapa tunakula mlo mmoja tangu juzi na jana chakula kisichokuwa na maji. Sasa haya ni mateso,” alisema John

Kuhusu gharama za nauli, Elias Maduka kutoka Simiyu alisema ili aweze kurudi nyumbani, anahitaji Sh60,000 lakini alipewa Sh45,000; wajumbe kutoka Mara walipewa Sh50,000 badala ya Sh70,000 na wale wa Kigoma Sh50,000 badala ya Sh80,000.

“Tulikopa nauli za kuja huku lakini wote hatukurudishiwa. Rais amesema hana fedha na hata posho baadhi wanasema waliweka rehani vitu vyao ili waweze kufika huku, jambo ambalo sasa hawajui watarudije na watalipaje madeni hayo,” alisema Maduka.

Kuhusu mkutano

Mjumbe kutoka Mkoa wa Simiyu, Gibasa John alisema mkutano huo haukuwa wa haki kutokana na fomu za kuomba uongozi kutogawiwa mikoani na badala yake zikatolewa siku moja kabla ya uchaguzi uliofanyika Juni 29. Katika uchaguzi huo nafasi za rais, makamu wake wa Bara na Zanzibar, katibu mwenezi na mipango, katibu wa vijana, katibu wa wazee na katibu wa wanawake zilikuwa na mgombea mmoja kila moja, jambo ambalo wajumbe hao walilipinga bila mafanikio.

No comments:

Post a Comment