Monday, 1 September 2014

Serikali ya Libya yakosoa matamshi ya Rais wa Uturuki....


Libya imesema imeshangazwa na matamshi ya Rais wa Uturuki kuhusu mahali panapofanyikia vikao vya bunge la wawakilishi la Libya na kueleza kuwa huko ni kuingilia masuala yake ya ndani. Wizara ya Mambo ya Nje ya Libya imetoa taarifa na kueleza kuwa, Rais Recep Tayyeb Erdogan wa Uturuki amekosoa kufanyika vikao vya bunge la Libya katika mji wa Tobruk. Wizara ya Mambo ya Nje ya Libya imesema kuwa kitendo hicho cha Rais wa Uturuki si sahihi bali ni uingiliaji wa wazi wa masuala ya ndani ya Libya. Wizara ya Mambo ya Nje ya Libya imeitaka serikali ya Uturuki itangaze iwapo matamshi hayo ya Erdogan ni msimamo rasmi wa Uturuki au ni msimamo binafsi wa rais huyo. Rais wa Uturuki alitoa matamshi hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya al Jazeera ya nchini Qatar. Itakumbukwa kuwa Rais Recep Tayyib Erdogan tarehe 17 mwezi Agosti  mwaka huu alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na Ageila Saleh Issa Spika wa bunge la Libya na akampongeza kwa kufanyika vikao vya bunge hilo huko Tobruk na kusisitiza kuwa bunge la Libya linatambuliwa kuwa marejeo pekee ya kisheria nchini humo na kwamba analiunga mkono bunge hilo. Ni vyema kuashiria hapa kuwa, bunge la Libya linaendesha vikao vyake katika mji wa Tobruk baada ya mji mkuu wa nchi hiyo Tripoli kukumbwa na machafuko yanayosababishwa na mapigano kati ya makundi ya wanamgambo.


HABARI NA GUDILA KULAYA
CHANZO:BBC SWAHILI

No comments:

Post a Comment