Sunday, 7 September 2014

SIMBA SC KUINGIA KAMBINI MBEZI BEACH KESHO

Na SALEHE ABDALA, 

SIMBA SC inaingia kambini kesho katika hoteli ya Shynovo, eneo la Africana, Mbezi Beach, Dar es Salaam kwa maandalizi ya mwisho ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Gor Mahia ya Kenya jana Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wachezaji wa Simba SC leo wamepewa mapumziko na kesho wataanza mazoezi Uwanja wa Boko Veterani.
Ijumaa wiki hii, Simba SC itasafiri hadi Mtwara kwa ajili ya mchezo wa kirafiki dhidi ya wenyeji Ndanda kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona Jumamosi jioni.
Mikono salama; Kipa namba moja wa Simba SC, Ivo Mapunda akiwaongoza wachezaji wenzake kuingia uwanjani jana dhidi ya Gor Mahia

Baada ya hapo, Wekundu hao wa Msimbazi watarejea Dar es Salaam kuendelea na maandalizi ya Ligi Kuu.
Kikosi cha kocha Mzambia, Patrick Phiri kimeonyesha kipo vizuri kuelekea Ligi Kuu, kutokana na kushinda mechi zake zote nne za majaribio.
Simba SC ilizifunga 2-1 Kilimani City, 2-0 Mafunzo na 5-0 KMKM, mechi zote zikipigwa Uwanja wa Amaan, Zanzibar kabla ya jana kuifumua 3-0 Gor Mahia. 
Ligi Kuu inatarajiwa kuanza Septemba 20, mwaka huu, mabingwa watetezi, Azam FC wakifungua dimba na Polisi Morogoro Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam Septemba 20, mwaka huu, wakati Yanga SC waliomaliza nafasi ya pili wataanza na Mtibwa Sugar Uwanja wa Jamhuri, Morogoro siku hiyo.
Washindi wa tatu, Mbeya City wataanza na JKT Ruvu ya Pwani, Uwanja wa Sokoine, Mbeya Septemba 20 na washindi wa nne Simba SC watafungua dimba na Coastal Union Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam Septemba 21.
Mechi nyingine za ufunguzi za Ligi Kuu zitakuwa kati ya Stand United watakaoikaribisha Ndanda ya Mtwara Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Mgambo JKT wataikaribisha Kagera Sugar Uwanja wa Mkwakwani, Tanga na Ruvu Shooting watakuwa wenyeji wa Prisons Uwanja wa Mabatini, Mlandizi mkoani Pwani.
Ikumbukwe ligi hiyo, itatanguliwa na mchezo wa Ngao ya Jamii Septemba 14 kati ya Azam FC dhidi ya Yanga kuashiria ufungzi rasmi wa msimu huo mpya wa ligi hiyo.PICHA KWA HISANI YA BIN ZUBEIRY

No comments:

Post a Comment