Habari
na Beatrice mbowe.
Msemaji wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Rajab Katimba
akizungumza na waandishi wa habari jana, kuhusu mambo mbalimbali ikiwa ni
pamoja na mchakato wa Katiba. Kulia ni Wajumbe, Shaban Ibrahim na Suleiman
Abdallah.
Jumuiya na
Taasisi za Kiislamu Tanzania imeungana na maaskofu mbalimbali kuwataka wajumbe
wa Bunge la Katiba kuheshimu Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa kwa mujibu wa
sheria na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Pia, taasisi hiyo
imemtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William
Lukuvi kujiuzulu nafasi zake zote za uongozi kutokana na kauli waliyodai ya
kichochezi, aliyoitoa katika Kanisa la Methodist, Jimbo la Dodoma kuwa
ukipitishwa muundo wa serikali tatu, jeshi litachukua nchi kwa sababu
itashindwa kuwalipa mishahara.
Akizungumza na
waandishi wa habari jana, Msemaji wa Jumuiya na Taasisi hizo, Sheikh Rajab
Katimba alilaani kauli kuhusu jeshi na kuwa makanisa yote yatafungwa na nchi
itakosa amani kutokana na kupitisha muundo huo wa serikali.
Sheikh Katimba alisema
Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa bungeni na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba imetokana na utafiti na uchambuzi wa
maoni ya wananchi wa Tanzania Bara na Visiwani ili kuboresha Muungano kutatua
kero zilizodumu kwa miaka 50 sasa.
Msimamo
Jumuiya hiyo iliweka
wazi msimamo wake wa kutaka serikali tatu na kutaka maoni ya makundi mbalimbali
ndani ya Bunge la Katiba kuheshimiwa.
Mjumbe wa Jumuiya hiyo,
Sheikh Ramadhan Sanze pia amesema si ustaarabu kwa kundi moja kuhodhi mchakato
kwa masilahi binafsi.
Alisema kukosoa maoni
ya waasisi wa Taifa si dhambi kwa sababu wao hawakuwa Mungu kwamba hawakosei,
badala yake amependekeza watu waachwe wazungumze kwa utashi wa matakwa yao juu
ya kile kilichowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
“Nchi hii haithamini
mchango wa wataalamu, tumeona Tume ilivyofanya kazi nzuri, leo hii wanatukanwa
hadharani, nawashangaa sana viongozi wa nchi hii,” alisema.
Sheikh Sanze amesema
miiko na misingi waliyoiweka waasisi wa Taifa inavunjwa na viongozi wenyewe
ambao leo wanasema waasisi wanatukanwa kwa kuwa wamependekeza serikali tatu
badala ya mbili walizounda waasisi.
“Kulikuwa na utaratibu
wa kubadilishana awamu za uongozi katika Serikali ya Muungano, awamu hii rais
akitoka Tanzania Bara, ijayo atatoka Zanzibar; hii ndiyo misingi waliyoiweka
waasisi, mbona leo haifuatwi? Huu ni unafiki...” alifafanua Sheikh Sanze.
Jumuiya hiyo imewataka wananchi wote kuendelea
na mshikamano katika kutengeneza Katiba Mpya yenye maridhiano na itakayoondoa
kero zilizodumu kwa zaidi ya miaka 50.
NB:Habari
hii waweza kupata kutoka mwananchi communication.