Tuesday, 12 August 2014

Dortmund na Bayern uso kwa uso leo Jumatano

Borussia Dortmund wanaikaribisha Bayern Munich Jumatano katika pambano la kujifaharisha kwa hadhi katika mchezo wa super cup nchini Ujerumani, huku kukiwa na vita vya maneno baina ya vilabu hivyo.

Borussia Dortmund Training
Borussia Dortmund wakifanya mazowezi
Borussia Dortmund inaikaribisha Bayern Munich katika kombe la Super cup nchini Ujerumani leo Jumatano , huku kukiwa na vita ya maneno baina ya vilabu hivyo vya juu nchini Ujerumani.

Matamshi ya mwenyekiti wa Bayern Munich Karl-Heinz Rummenigge kuhusiana na maelezo ya mkataba wa mshambuliaji nyota wa Dortmund Marco Reus hayajawafurahisha viongozi wa Dortmund muda mfupi kabla ya pambano hilo la kufungua pazia la msimu mpya wa 2014-15 nchini Ujerumani.
Fußball Bundesliga 30. Spieltag FC Bayern München - Borussia Dortmund
Mpambano kati ya Byern Munich na Borussia Dortmund












Dortmund inahofu kuwa Bayern iko mbioni kumvutia mchezaji huyo kwenda kwa mahasimu wao wakubwa upande wa kusini mwa Ujerumani kupitia kifungu cha kitoka nyumba baada ya kumnyakua Mario Goetze mwaka 2013 na Robert Lewandowski mwaka huu kutoka klabu hiyo.

Mkurugenzi wa spoti wa Dortmund Michael Zorc amesema wazi kuwa Rummenigge anapaswa kufunga "domo lake mara moja ," lakini mkurugenzi wa spoti wa Munich Matthias Sammer , mchezaji wa zamani wa Borussia Dortmund amesisitiza kuwa na hapa namnukuu, "hatutanyamazishwa na yeyote."
Bayern na Dortmund ni vilabu vikubwa bila shaka katika soka la Ujerumani. Dortmund ilishinda ligi mwaka 2011 pamoja na kunyakua mataji yote mawili nchini humo mwaka 2012 ,ambapo Bayern ilijibu kwa kunyakua mataji matatu katika msimu mmoja wa 2013 na mataji mawili nchini Ujerumani msimu uliokwisha.
Bayern iliishinda Dortmund kwa mabao 2-1 katika super cup mwaka 2012 wakati Dortmund iliikandika Bayern mabao 4-2 katika mchezo kama huo msimu uliopita.
Siku ya Jumatano ambapo pambano hilo litafanyika mjini Dortmund , mwenyekiti wa Bayern Karl-Heinz Rummenigge ameshasema kuwa chochote kitakachotokea katika pambano hilo hakitakuwa na uzito mkubwa kwa kuwa timu zote hazijafikia katika kiwango cha juu cha mchezo wao bado. CHANZO DW
 HABARI NA CHARLES B. CHAMI 

No comments:

Post a Comment