Wednesday, 13 August 2014

WATU 114 WAULIWA NA BOKO HARAMU NCHINI NIGERIA

 
HABARI NA 
   JESCA MHOKA
Zaidi ya watu 100 wakiwemo wanajeshi kadhaa wa serikali, wameuawa katika mapigano yaliyozuka kati ya jeshi la nchi hiyo na wanamgambo wa Boko Haram katika jimbo la Borno, kaskazini mwa Nigeria. Jeshi la serikali limetangaza leo kwamba, mapigano hayo yaliibuka jana wakati askari wa nchi hiyo walipokuwa katika doria kwenye mji wa
Gwoza ambao umekuwa ukidhibitiwa kwa zaidi ya wiki mbili na kundi la kigaidi la Boko Haram. 
Mji huo uko umbali wa takriban kilomita 135 kaskazini mwa mji wa Borno ambao ni makao makuu ya jimbo la Maiduguri. Katika tukio jingine, wanachama wa kundi hilo wamevishambulia vijiji viwili vya Wakristo katikati mwa Nigeria. Wakazi wa vijiji hivyo wamesema leo kuwa, wanachama wa Boko Haram walishambulia vijiji vya Babayo na Yalwa vya mji wa Jos katika jimbo la Plateau katikati mwa Nigeria na kuua watu wasiopungua 14 na kupora mifugo yao.

 Emmanuel Ebo, afisa uhusiano wa umma wa idara ya polisi ya jimbo hilo amethibitisha tukio hilo. Hii ni katika hali ambayo maeneo ya kaskazini na katikati mwa Nigeria yamegeuka kuwa uwanja wa mapigano kati ya wafugaji wa kabila la Fulani ambao wengi wao ni Waislamu na wanakijiji wa Kikristo, mapigano ambayo yanatokana na ugomvi wa ardhi.
CHANZO:IDHAA YA KISWAHILI YA TEHRAN

No comments:

Post a Comment